Waathiriwa wa mafuriko Nairobi wapatiwa msaada

Waziri Ruku na viongozi aliokuwa nao waliwapa wakazi hao chakula, magodoro, vifaa vya jikoni na vifaa vya usafi.

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Utumishi wa Umma, Maendeleo ya Rasilimali Watu na Mipango Maalum, Geoffrey Kiringa Ruku leo alizuru eneo la Drive-In, Wadi ya Utalii, Eneo Bunge la Ruaraka, kaunti ya Nairobi.

Akiwa ameandamana na Katibu wa Mipango Maalum Ismael Maalim na Mbunge wa eneo hilo TJ Kajwang’ waziri alitagusana na familia zilizoathirika na mafuriko na maporomoko ya ardhi katika eneo hilo huku akigawa msaada.

Mama mmoja na watoto wake wawili wakazi wa eneo hilo walifariki kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jana.

Angalau familia 55 katika eneo hilo zimeathirika na mafuriko baada ya nyumba zao kuharibiwa.

Kama sehemu ya mwitikio wa dharura kupitia Idara ya Mipango Maalum chini ya Wizara ya Utumishi wa Umma, Maendeleo ya Rasilimali Watu na Mipango Maalum, serikali iliwasilisha msaada kwa watu hao.

Waligawiwa chakula, magodoro, vifaa vya jikoni na vifaa vya usafi.

Katika juhudi za kutafuta suluhisho la kudumu kwa maporomoko ya ardhi na mafuriko, Waziri Ruku alimwagiza Katibu wa Mipango Maalum kuitisha kikao cha haraka cha mashirika mbalimbali kikihusisha Serikali Kuu na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kujadili hatua za kukabiliana na hali hiyo ili kulinda maisha ya watu wa eneo hilo na mali zao.

Waziri RUKU alisisitiza dhamira ya serikali ya kuchukua hatua za tahadhari na kujitayarisha mapema kwa dharura kwa kushirikisha wadau wote husika ili kuhakikisha miundombinu muhimu kama mifereji ya maji kwenye barabara kuu ya Thika na katika makazi yasiyo rasmi iko katika hali bora ili kuzuia vifo na uharibifu wa mali.

Share This Article