Kenya imetoa wito kwa nchi za Afrika kufikiria upya na kuboresha huduma zao za posta ili kunufaika na fursa zinazoletwa na mabadiliko ya kidijitali na ongezeko la biashara ya mtandaoni.
Ujumbe huu ulitolewa waziri wa mawasiliano na uchumi dijitali nchini Kenya katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na katibu wa utangazaji Stephen Isaboke, katika ufunguzi rasmi wa Kongamano la viongozi wa udhibiti wa Posta Afrika.
Akihutubia viongozi wa posta, wasimamizi wa sekta hiyo na wadau wa kimataifa katika Hoteli ya Sarova Panafric jijini Nairobi, Isaboke alisisitiza nafasi muhimu ya sekta ya posta katika kuunganisha jamii, kuchochea ukuaji wa uchumi, na kuboresha upatikanaji wa huduma za serikali.
Alisema kuwa, licha ya uwezo wake mkubwa, sekta ya posta barani Afrika bado haijafikia kiwango inachostahili na inahitaji mageuzi ya muundo ili kufungua uwezo wake wa kiuchumi.
“Kwa mfumo wa posta ulioboreshwa ipasavyo, sekta hii inaweza kuchangia karibu asilimia 7 ya Pato la Taifa” alisema Isaboke akinukuu utafiti wa UPU.
Alirejelea pia ripoti ya mwaka 2023 iliyoonyesha kuwa zaidi ya barua bilioni 1.2 zilichakatwa barani Afrika, ishara ya umuhimu wa sekta hiyo katika enzi hii ya kidijitali.
Alihimiza serikali za Afrika na mashirika ya posta kuchangamkia soko la biashara ya mtandaoni duniani ambalo linakadiriwa kufikia dola trilioni 4.32 kufikia mwaka 2025, akibainisha kuwa Afrika kwa sasa inachangia chini ya asilimia 3 ya mapato hayo.
“Hii ni fursa ya dhahabu ambayo hatufai kupoteza,” aliongeza, akitaja uwezekano wa kuwa na watumiaji wa biashara mtandaoni milioni 500 barani Afrika kufikia mwisho wa mwaka 2025.
Kwa upande wa Kenya, Bw. Isaboke alieleza mageuzi kadhaa yanayoendelea, kama mswada wa Mfumo wa Kitaifa wa Anwani na Mkakati wa Kitaifa wa Biashara Mtandaoni wa Kenya, unaolenga kuboresha miundombinu ya usambazaji hadi ngazi ya mwisho na biashara ya kidijitali.
Aidha, alipongeza Shirika la Posta Duniani (UPU) kwa kuendelea kusaidia juhudi za Kenya, likiwemo pendekezo la hivi karibuni la msaada wa Franka za Uswizi 150,000 kwa ajili ya kuimarisha mpango wa Post4Health nchini Kenya.
“Tukiwa tunapanga njia mpya kwa sekta ya posta ya Afrika, hebu tulinganishe sera za TEHAMA, tukumbatie ubunifu, na tujitoe kujenga mifumo thabiti, kijani na jumuishi,” alihimiza.
Kongamano hili, lililohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa UPU Bw. Metoki Masahiko, Katibu Mkuu wa PAPU Dkt. Sifundo Chief Moyo, pamoja na wadau wengine muhimu, linatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa udhibiti wa huduma za posta barani Afrika.