Papa Francis alipozuru Afrika

Papa alizuru Afrika miaka ya 2015, 2017, 2019 na 2023.

Marion Bosire
2 Min Read

Katika ziara yake ya kwanza kabisa barani Afrika, kiongozi aliyefariki hivi punde wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis alichagua kuanza na Kenya.

Ziara hiyo ilikuwa ya mataifa matatu ambayo ni Kenya, Uganda na Central African Republic.

Papa Francis alipokutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda

Francis aliwasili Kenya Novemba 25, 2015 ambako alikaa kwa siku tatu hadi Novemba 27, 2015 na ndiye kiongozi wa pili wa kanisa katoliki ulimwenguni kuwahi kuzuru Kenya, baada ya John Paul wa pili ambaye alizuru Kenya mara tatu.

Alifanya mkutano na Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta, viongozi wa kanisa katoliki nchini, akaandaa misa ya wote katika uwanja wa chuo kikuu cha Nairobi kabla ya kuzuru mtaa wa Kangemi.

Papa Francis alipokutana na Rais wa CAR

Mwaka 2017, Papa Francis alirejea barani Afrika ambapo alizuru jiji la Cairo nchini Misri na 2019 akazuru Morocco.

Safari yake ya hivi punde kabisa ya Afrika ni ya Januari 2023 ambapo alizuru Congo na Sudan Kusini.

Ujio wake katika bara hili ulichochewa na haja ya kutambua ukuaji wa umuhimu wa kanisa katoliki barani, kuangazia masuala kama amani na haki ya kijamii na kukuza mazungumzo na mshikamano.

Papa Francis ameaga dunia leo Jumatatu Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88 baada ya kuugua homa ya mapafu iliyosababisha alazwe hospitalini kwa muda.

Share This Article