Hospitali zazidiwa na visa vya maradhi ya Chikungunya katika kisiwa cha Reunion

Idara ya huduma za afya katika kisiwa hicho ilisema kuwa mlipuko huo unaongezeka ambapo Kila siku wanapokea wagonjwa kati ya 30 na 40 wenye chikungunya.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkuu wa huduma ya hospitali katika kisiwa cha Reunion cha Ufaransa katika Bahari Hindi ametoa wito wa msaada wa kitabibu ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa chikungunya unaosambazwa na mbu.

“Tumelemewa kabisa” alisema Lionel Calenge kupitia kituo cha redio cha RMC, akiongeza kwamba wataalamu wa milipuko ya magonjwa walitabiri kilele cha mlipuko kufikia katikati ya Aprili na sasa kimejiri.

Wito wake umetolewa siku moja kabla ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuanza ziara ya siku tano katika maeneo ya Ufaransa ya Bahari ya Hindi, ikiwa ni pamoja na Reunion ambapo atakuwa Jumanne.

Tangu mwanzo wa mwaka huu, chikungunya imeua watu sita kisiwani humo na inakadiriwa kwamba mtu mmoja kati ya tisa ameathiriwa kati ya wakazi wapatao 900,000 wa kisiwa hicho.

Hata ingawa huduma ya afya ya umma ya Ufaransa ilisema kuwa mlipuko huo unaonekana kupungua mapema Aprili, Calenge alisema Kila siku wanapokea wagonjwa kati ya 30 na 40 wenye chikungunya katika wadi mbili tu za dharura.

Hospitali nne anazosimamia hazina vitanda vya kutosha na watu 581 wamelazwa hospitalini kutokana na ugonjwa huo tangu mwanzo wa mwaka 2025, wakiwemo watoto wachanga 46.

Wahudumu wa afya 540 wako likizo ya ugonjwa tangu mapema mwezi Machi kwa sababu ya kuambukizwa chikungunya, kulingana na Calenge.

Alisema hadi sasa huduma wamepokea madaktari watatu wa msaada, lakini wanahitaji wengine sita.

Idara ya huduma za hospitali katika kisiwa hicho imeahirisha takriban upasuaji 300 uliopangwa awali na kuwaita wafanyakazi waliokuwa likizo ili kukabiliana na mlipuko huo.

Share This Article