Wakazi wa Soko Mjinga huko Isiolo wanakadiria hasara baada ya Pasaka yao kuvurugwa na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na kuathiri angalau nyumba 200.
Mvua hiyo ambayo haijashuhudiwa kwa muda mrefu katika eneo la Isiolo ilisababisha uharibifu mkubwa wa mali ya mamilioni ya pesa na kuwaacha baadhi ya wakazi bila makao.
Watu watatu akiwemo mtoto mdogo wanahofiwa kufariki kutokana na mafuriko hayo huku wengine wawili wakisombwa na gari ambayo ilikuwa imebeba watu watatu, mmoja akifanikiwa kujiokoa na gharika ya mafuriko hayo.
Lucia Manyara ambaye ana matatizo ya afya na mkazi wa mtaa wa Soko mjinga alisimulia matukio ya usiku huo wa mvua kubwa, ya jinsi vijana walivyomuokoa wakati nyumba yake ilipozamishwa na mafuriko akiwa ndani. Kulingana na Lucy tangu aanze kuishi katika eneo hilo zaidi ya miaka 40 iliyopita alipokuwa msichana mdogo, hajawahi kuona maji mengi ya mvua kama aliyoshuhudia.
Wakazi hao wametoa wito kwa serikali ya Kaunti na ile ya Kitaifa kuingia kati na kuweka mikakati ambayo itazuia mkasa kama huo wakati mwingine.
Hata Hivyo, wanataka uboreshwaji wa daraja la Soko Mjinga ufanywe na mifumo ya kupitisha maji itengenezwe vizuri.