Kenya na Ethiopia zimetia saini mkataba wa ushirikiano katika utekelezaji wa eneo la biashara huru Barani Afrika.
Mataifa hayo mawili yametia saini mkataba wa makubaliano, utakaoharakisha utekelezaji wa eneo huru la kibiashara Barani Afrika baina ya Kenya na Ethiopoia, kupitia mfumo bora wa kibiashara uliorahisishwa.
Akizungumza mjini Mombasa, Waziri wa Uwekezaji, Biashara na ustawi wa Viwanda Lee Kinyanjui, alisema serikali za mataifa hayo mawili zitaharakisha biashara eneo la mpakani, kufuatia changamoto zinazoshuhudiwa kati ya jamii za mpakani zinazoishi Moyale nchini Kenya.
Kinyanjui alidokeza kuwepo kwa changamoto kadhaa, na hivyo ipo haja ya makubaliano hayo, ili kuhakikisha jamii zinazoishi mpakani zinafanya biashara kwa njia huru.
“Tunasisitiza kwamba Kenya na Ethiopia zitatafuta njia za kutekeleza biashara huru, ili bidhaa zinazozalishwa Kenya au Ethiopia zitafika katika soko na kwamba raia wa nchi hizo mbili wanaweza fanya kazi katika mataifa hayo bila kusahau utalii Mombasa na shughuli zingine za kuimarisha chumi zetu,’ alisema Kinyanjui.
Kwa upande wake, waziri wa biashara na ujumuishaji wa kikanda wa shirikisho la kidemokrasia la Ethiopia Kassahun Gofe, alisisitiza umuhimu wa kuhitimisha mazungumzo, ili kuanza utekelezaji wa utaratibu wa biashara uliorahisishwa ili kuharakisha biashara kati ya jamii zinazoishi katika mipaka ya nchi hizo mbili.