Wafanyabiashara na wakazi wa Kagio, eneo bunge la Ndia , kaunti ya Kirinyaga, wamepongeza upanuzi wa soko la kisasa la Kagio, unaotarajiwa kumaliza changamoto ya msongamano.
Ujenzi wa soko hilo la gorofa mbili, unatekelezwa na serikali ya kaunti hiyo kwa ushirikiano na serikali ya taifa, chini ya mpango wa kufufua uchumi.
Upanuzi wa soko hilo ni mojawepo wa miradi iliyozinduliwa na Rais William Ruto wiki mbili zilizopita wakati wa ziara yake ya maendeleo katika eneo la Mlima Kenya.
Soko hilo la kisasa litakalogharimu kitita cha shilingi milioni 357, litakuwa na vifaa kama vile uunganishwaji kwenye intanet, vyoo, usambazaji maji wa kutegemewa, ua wa ukuta na upatikianaji wa nguvu za umeme.
Huku idadi ya wafanyabiashara ikiongezwa kutoka 1,500 hadi 3,000, ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka 2026.