Mwanamume akamatwa kwa kumdhulumu kimapenzi mtoto wa umri wa miaka 14

Tom Mathinji
2 Min Read
Mwanamume akamatwa Homa Bay kwa madai ya dhuluma za kimapenzi.

Mwanamume wa umri wa miaka 36 amekamatwa kwa madai ya kumdhulumu kimapenzi mtoto wa umri wa miaka 14 katika kaunti ndogo ya Ndhiwa kaunti ya Homa Bay.

Kulingana na naibu wa Chifu wa kata ndogo ya Goyo Enos Nyawade , mwanamume huyo alikamatwa katika kijiji cha Maseje baada ya malalamishi kutoka kwa wananchi.

Mwanamume huyo anadaiwa kumhadaa msichana huyo kwa kumpa pesa na kwamba amekuwa akifanya uovu huo tangu mwezi Disemba mwaka jana.

“Uchunguzi wetu wa awali umebaini kuwa mwanamume huyo amekuwa akimdhulumu mtoto huyo tangu mwezi Disemba mwaka 2024,” alisema Nyawade.

Anadaiwa kwenda mafichoni baada ya kugundua kuwa alikuwa akitafutwa kutokana na uovu huo.

“Ametupatia wakati mgumu wa kumtafuta baada ya kuenda mafichoni, alipogundua tulikuwa tunamtafuta,” aliongeza naibu huyo wa chifu.

Baada ya kukamatwa mwanamume huyo alikabidhiwa maafisa wa polisi ambao wanamzuia, akisubiri kufikishwa mahakamani.

Nyawade alimtaja mwanamume huyo kuwa na tabia ya dhuluma za kimapenzi licha ya kwamba amewaoa wake wengi.

“Mwanamume huyo amewaoa wake wengi na bado anawadhulumu wasichana kimapenzi,” alidokeza mwanamume huyo.

Mtawala huyo alitoa wito kwa wazazi kuwachunga wasichana wao, huku akitoa onyo kali kwa wale wanaowadhulumu wasichana wenye umri mdogo.

“Tunapaswa kusimama kidete kwa kulinda haki za wasichana wetu. Bila kufanya hivyo tutakosa viongozi wa kike siku zijazo,” alisema Nyawade.

TAGGED:
Share This Article