Mwanamuziki tajika wa Uganda Jose Chameleone alirejea nchini humo baada ya kukaa Marekani kwa zaidi ya miezi mitatu kwa ajili ya matibabu.
Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kuwasili, mwimbaji huyo alizungumzia maradhi yake kwa mara ya kwanza.
Hapo ndipo alikiri kwamba anaugua ugonjwa wa kongosho almaarufu Pancreatitis, na anaendelea kupokea matibabu.
Kuhusu kilichomsababishia ugonjwa huo, Chameleone alitaja walichosema madaktari ambacho ni mtindo wa maisha huku akipuunza madai kwamba kisababishi cha pekee ni pombe.
“Visababishi ni vingi kama vile msongo wa mawazo, msimbojeni na ukosefu wa usingizi.” alisema Chameleone akiongeza kwamba watu waliangazia tu unywaji pombe lakini kukosa kupumzika na kula vizuri pia ni visababishi.
Mmiliki huyo wa kampuni ya muziki ya Leone Island alisema kwamba wakati alipelekwa Marekani kwa matibabu, kongosho yake ilikuwa imeharibika kiasi cha kutoweza kutoa vimeng’enya vya kusaga chakula.
Mwezi Februari, madaktari walimfanyia upasuaji wa kuondoa sehemu iliyokuwa imeathirika vibaya ya kiungo hicho na baadaye akapatiwa dawa aina ya Creon ambazo hutekeleza wajibu wa kongosho mwilini.
Chameleone alielezea kwamba dawa hizo ni ghali mno ambapo kipimo cha miezi mitatu tu kinagharimu dola elfu nane.
Jumatatu wiki ijayo, familia yake itaandaa hafla ya maombi ya kutoa shukrani katika parokia ya Lweza.