Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki EALA, ambaye pia alikuwa Seneta mteule Falhada Dekow amepigwa marufuku kuingia katika majengo ya bunge kwa muda wa siku 90.
Adhabu hii ilitolewa na Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula leo alasiri, baada ya video kusambazwa mitandaoni ikionyesha Dekow na mbunge mteule Umulkheir Harun Mohamed wakipigana bungeni jana.
Kawaida bunge huwa linaruhusu waliokuwa wabunge na wabunge wa EALA kufika katika maeneo fulani ya majengo ya bunge bila kizuizi.
Katika uamuzi wake, Spika Wetangula alisema wabunge ni lazima wabunge wadhihirishe nidhamu ya hali ya juu wanapokuwa katika majengo ya bunge kinyume na walivyofanya wawili hao.
Huku akielezea kwamba suala hilo lilistahili kuwasilishwa kwa kamati ya bunge kuhusu mamlaka na fadhila ili iliangazie na kutoa mapendekezo Spika Wetangula alisema kwamba aliamua kumpa Umulkheir fursa ya kujieleza na kuomba msamaha.
Kwa upande mwingine, Wetangula alisema Deko ambaye hana fursa ya kujieleza mbele ya bunge anatakiwa kufanya hivyo kwa kumwandikia waraka Spika wa bunge.
Alisema pia kwamba haruhusiwi kuingia bunge kwa siku 90 isipokuwa siku ambayo atawasilisha maelezo na msamaha kwa spika na atatakiwa kuandamana na walinzi wa bunge.
Katika maelezo yake, Umulkheir ambaye mkono wake ulikuwa umefungwa kama ambao uliumia alisema hakutarajia mazungumzo yake na Dekow yangeishia katika vita.
Anasema alitaka kujua kutoka kwa Dekow sababu ya kumdhalilisha kila mara mitandaoni na badala ya kujibu Deko aliamua kumrushia kikombe cha chai.
Spika Wetangula aliashiria kwamba atawajibisha aliyerekodi na kusambaza video hiyo mitandaoni na kulingana na Umulkheir, mbunge wa Tigania Mashariki Mpuru Aburi ndiye pekee alionekana akirekodi kisa hicho.