USAID: Makali ya kusitishwa kwa msaada yahisiwa zaidi kaskazini mwa Kenya

Martin Mwanje
4 Min Read
Maafisa wa hospitali wakikagua makasha ya mwisho ya dawa zilizowasilishwa na shirika lililovunjwa la USAID (Picha kwa hisani ya Luis TATO / AFP)

Katika kaunti kubwa na maskini zaidi nchini Kenya, hali ya kukata tamaa ya mkurugenzi wa hopitali moja katika kaunti hiyo inadhirika wakati akielezea kuwa kusitishwa kwa msaada unaofadhiliwa na Marekani kuna maana kwamba hospitali yake itapungukiwa na dawa za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) mwezi ujao. 

“Kuanzia wakati huo na kuendelea mbele, sijui,” Ekiru Kidalio alisema, akielezea hofu juu ya ukosefu wa tiba ya surua na VVU (HIV) miongoni mwa mambo mengine.

Kaunti ya Turkana inayopatikana kaskazini kabisa mwa Kenya inapakana na Ethiopia, Sudan Kusini na Uganda na ina wakazi wanaokaribia milioni moja. Hii ni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2019. Theluthi moja kati yao ni wakimbizi wanaotegemea msaada wa kigeni.

Utawala wa Rais Donald Trump umetangaza upunguzaji wa ufadhili mkubwa kwa USAID ambayo bajeti yake ya kila mwaka ni takriban dola bilioni 43, ambayo ni zaidi ya asilimia 40 ya msaada wa kibinadamu kote duniani.

Uamuzi huo, uliofanywa umbali wa maelfu ya kilomita mjini Washington, tayari unaanza kuhisiwa katika hospitali ya rufaa ya Lodwar katika kaunti ya Turkana, amesema Kidalio ambaye ni kaimu mkurugenzi wa hospitali hiyo.

USAID iliwaajiri wafanyakazi 64, wakiwemo wauguzi na maafisa wa kliniki, kati ya wafanyakazi wapatao 400 hospitalini hapo.

“Wafanyakazi hao wote walifutwa kazi,” alisema.

“Kila kitu kilisimamishwa… na kisha dawa hazikupokelewa,” aliongeza Kidalio, akielezea wasiwasi hasa juu ya uhaba wa chanjo ya surua.

Kidalio amesema “hakufahamu” mipango yoyote ya serikali ya Kenya kukabiliana na uhaba huo.

Gavana wa kaunti ya Turkana Jeremiah Lomorukai alitoa wito wa kurejeshwa kwa mipango inayofadhiliwa na USAID wakati kaimu Balozi wa Marekani nchini Kenya Marc Dillard alipotembelea kaunti hiyo wiki jana.

“Kuna wasiwasi mkubwa kwa sababu Marekani imesitisha msaada,” Lydia Muya mwenye umri wa miaka 32 ambaye ni mkazi wa kaunti hiyo aliiambia AFP.

“Tunaona hiyo sasa kuwa hatari kubwa kwetu, kwa sababu tunategemea dawa hizo, kwa hivyo watu wengi watateseka,” aliongeza Muya.

“Hali ni ngumu zaidi.”

‘Nitakula vip?’

Taswira hiyo inazidi kuwa mbaya zaidi katika kambi ya Kakuma wanamoishi watu zaidi ya 300,000 hasa kutoka nchi za Sudan Kusini,  Somalia, Burundi na Rwanda.

Maandamano yalizuka kambini hapo mwezi jana baada ya kuibuka kwa taarifa kuwa mgao, ambao tayari ulipunguzwa mwaka jana, utapunguzwa zaidi kwa sababu ya kupunguzwa kwa matumizi ya msaada wa kigeni wa USAID.

“Hali ilikuwa tete,” alisema mfanyakazi mmoja wa kutoa misaada, ambaye amehudumu huko Kakuma kwa karibu miaka mitano, ambaye hakutaka kutambuliwa kwa sababu haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.

Alipoulizwa ikiwa bidhaa za msaada zinawasili, jibu lake lilikuwa bayana: “La. Na pesa zipi? Hakuna ufadhili, hakuna wafanyakazi.

Alikadiria kuwa takriban asilimia 40 ya wafanyakazi tayari wamefutwa kazi kutokana na hatua ya Marekani kusitisha msaada.

Hali inaweza ikawa mbaya zaidi.

Mpango wa Chakula Duniani (WFP), unaounga mkono wakimbizi wa Kakuma wanaokaribia 200,000, uliiambia AFP kuwa umepunguza mgao, unaowasilishwa kama chakula na pesa taslimu, hadi asilimia 40 ya kiwango chao cha awali.

Mama wa watoto wanne ambaye ameishi kambini hapo kwa karibu miongo miwili, aliiambia AFP kuwa ana hofu.

“Nitakula kwa siku ngapi? Chakula kinaweza kumalizika haraka zaidi,” alisema, akiomba kutotambulishwa kwani hana uhakika ikiwa anaruhusiwa kuzungumza na wanahabari.

“Trump amesimamisha kila kitu, na kumefungwa sasa, hakuna kitu kinachoingia na hakuna kitu kinachotoka nje.”

Share This Article