Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi amepuuzilia mbali ripoti za vyombo vya habari zinazomhusisha na chama kipya akisema kwamba yeye yuko chini ya chama cha muungano wa Kenya Kwanza.
Haya yanafuatia uzinduzi wa chama kilichopatiwa jina la Umoja Summit Party – USP, miezi kadhaa baada ya chama chake cha ANC kumezwa na Kenya Kwanza.
Chama cha USP kilizinduliwa na wanasiasa wanaoaminika kuwa marafiki wa Mudavadi na ambao wanaaminika kuelekezwa naye kuzindua chama hicho.
USP kilizinduliwa siku tatu zilizopita ambapo Barack Muluka ni katibu mkuu, Naomi Saidi ni naibu wake na kiongozi wa chama ni Godfrey Kanoti.
Mudavadi hata hivyo amesema kwamba katika muda wote ambao amejuhusisha na siasa, ameshikilia uadilifu, uaminifu na heshima kama mtindo wake wa kufanya mambo na wala sio kuwa ndumakuwili.
Mkurugenzi wa mawasiliano katika afisi ya Mudavadi Jacob Ng’etich, alisema waziri huyo anaamini katika umoja na utangamano na hatua yake ya kukubali chama cha ANC kumezwa na kile cha UDA ni wa hiari na uliungwa mkono na wanachama.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba Mudavadi amejitolea kwa jukumu la serikali la kutumilia wakenya kwa bidii na hana nia kamwe ya kujiunga na chama kingine.