Rais Ruto akutana na viongozi wa magharibi Ikulu

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto alipokutana na viongozi wa magharibi katika Ikulu ya Nairobi
Rais William Ruto leo Jumatano amekutana na viongozi kutoka eneo la magharibi mwa nchi katika Ikulu ya Nairobi. 
Viongozi hao walijumuisha Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula na Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Magavana Paul Otwoma wa Busia, Ken Lusaka wa Bungoma na Fernandes Barasa wa Kakamega, wabunge na Waziri wa Afya Dr. Deborah Barasa pia walihudhuria mkutano huo.
Rais Ruto anasema anashiriki mazungumzo na viongozi kutoka kote nchini kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo bila kuacha nyuma eneo lolote.
Wakati wa mkutano kati yake na viongozi hao, Rais Ruto anasema walipigia darubini hatua iliyopigwa katika utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa uzalishaji wa chakula, hususan kuongeza ugavi wa mbolea kwa wakulima ili kuboresha uzalishaji wa chakula.
Aidha, suala la kufufua sekta ya sukari na kahawa katika eneo la magharibi lilijadiliwa.
Masuala mengine yaliyopewa kipaumbele wakati wa mkutano huo ni uboreshaji wa dharura wa miundombinu ikiwa ni pamoja na barabara, uunganishaji umeme na upatikanaji wa afya ya umma.
Rais Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa hakuna eneo lolote nchini litakaloachwa nyuma katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali ili kukagua miradi ya maendeleo, na amepangiwa kufanya ziara katika eneo la Mlima Kenya hivi karibuni.
Share This Article