Mia Love ambaye aliandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mweusi aliyechaguliwa kama mbunge wa chama cha Repulican nchini Marekani amefariki akiwa na umri wa miaka 49.
Familia yake ilitumia akaunti yake ya X kutangaza kifo cha mwakilishi huyo wa zamani wa eneo la Utah, Jumapili Machi 23, 2025.
“Kwa nyoyo za shukrani zilizojawa na athari ya kipekee ya Mia katika maisha yetu, tunataka mfahamu kwamba alifariki kwa amani.” ulisema ujumbe huo wa familia yake.
Watu wa familia yake waliendelea kwa kushukuru wote ambao wamekuwa wakiwatumia jumbe za pole, wakiwaombea na kuwatakia mema.
Love alikuwa anaugua saratani ya ubongo na alikuwa anapokea matibabu katika chuo kikuu cha Duke.
Gavana wa Utah alimwomboleza Love akimtaja kuwa rafiki wa kweli. Alisema pia kwamba urithi wake wa huduma kwa watu wa Utah uligusa wengiambao walimfahamu.
Love alianza taaluma yake ya uanasiasa mwaka 2003, wakati aliibuka mshindi wa uchaguzi wa mwakilishi katika manispaa huko Saratoga Springs.
Baadaye alihudumu kama meya wa jiji hilo kabla ya kushindwa kwenye uchaguzi wa mwakilishi wa bunge na Jim Matheson wa chama cha Democrat.
Mwaka 2014, Love alishinda kwenye uchaguzi na kuwa mwanamke wa kwanza mweusi wa chama cha Republican kuwahi kushinda uchaguzi kama mbunge wa bunge la Congress.
Alihudumu kwa mihula miwili kabla ya kushindwa kwenye uchaguzi mwaka 2018 na Ben McAdams wa chama cha Democratic.