Ajali ya ndege ambayo ilitokea katika eneo la Ceel Xabaaloow, umbali wa kilomita 24 kusini magharibi mwa Mogadishu jana ilisababisha vifo vya watu watano waliokuwemo.
Mamlaka ya uchukuzi wa ndege nchini Somali, Somali Civil Aviation Authority (SCAA), imethibitisha ajali hiyo ya ndege aina ya Buffalo DHC-5D, nambari tambulishi 1O9 na nambari ya usajili 5Y-RBA.
Kulingana na ripoti za mwanzo, ajali hiyo ya ndege ya kampuni ya Trident Aviation ilitokea Jumamosi, Machi 22, 2025 jioni saa 11 na dakika 43.
Ndege hiyo ilikuwa imeondoka uwanja wa ndege wa Dhobley na ilikuwa ikielekea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Abdulle jijini Mogadishu wakati ajali ilitokea.
Majina ya wahasiriwa wa ajali hiyo bado hayajawekwa wazi lakini SCAA ilithibitisha kwamba abiria wote pamoja na wahudumu walifariki.
Mashirika ya serikali na washirika wengine tayari wametuma makundi ya wataalamu hadi eneo la tukio, ingawa kilichosababisha ajali hiyo bado hakijabainika.
“Tunatoa rambirambi zetu kwa familia na wapendwa wa walioangamia katika ajali hii.” ilisema mamlaka ya SCAA katika taarifa kwa vyombo vya habari.
SCAA imeahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu mkasa huo punde zitakapojiri huku ikiahidi kutekeleza uchunguzi wa kina kwa ushirikiano na serikali ili kung’amua kilichosababisha ajali hiyo.