Kiongozi wa Hamas auawa katika mashambulizi ya Israel

Haya yanajiri siku moja baada ya mashambulizi kadhaa ya mabomu yaliyotekelezwa na jeshi hilo la Israel kusababisha vifo vya wapalestina 34

Marion Bosire
2 Min Read

Jeshi la Israel linaendeleza mashambulizi katika ukanda wa Gaza, mashambulizi ambayo yamesababisha vifo vya wengi akiwemo kiongozi wa kundi la Hamas Salah al-Bardawil huko Khan Younis.

Haya yanajiri siku moja baada ya mashambulizi kadhaa ya mabomu yaliyotekelezwa na jeshi hilo la Israel kusababisha vifo vya wapalestina 34.

Kando na Gaza, jeshi la Israel linashambulia pia eneo la Kusini mwa Lebanon kufuatia shambulizi la roketi na kuua takribani watu saba, hatua inayohatarisha hata zaidi mkataba wa kusitisha vita.

Mkataba huo uliafikiwa na kundi la Hezbollah miezi minne iliyopita.

Wizara ya afya ya Gaza inaripoti kwamba kufikia sasa wapalestina 49,747 wameuawa na wengine 113,213 kujeruhiwa tangu Israel ilipoanza kushambulia Gaza huku afisi ya vyombo vya habari ikiweka idadi ya vifo kuwa 61,700.

Idadi hiyo mpya ya vifo ni kutokana na wapalestina wengi wasiojulikana walipo hadi sasa na wanaaminika kufa chini ya vifusi.

Watu 1,139 wanaaminika kuuawa nchini Israel katika shambulizi la kundi la Hamas la Oktoba 7, 2023, huku wengine zaidi ya 200 wakishikwa mateka.

Shambulizi hilo ndilo lilizua vita katika ukanda wa Gaza katika kile ambacho Israel ilikitaja kuwa kulipiza kisasi.

Mkataba wa kusitisha mapigano Gaza uliafikiwa na kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu wa 2025 na awamu ya pili ya mpango huo ilistahili kuanza baada ya mazungumzo.

Lakini Israel imerejelea mashambulizi yake Gaza kama njia ya kushinikiza kundi la Hamas liachilie mateka wa Israel waliosalia.

Share This Article