Mwanamuziki wa Tanzania Gift Stanford Joshua maarufu kama Gigy Money amezindua kibao kwa jina “Nimenasa” ambacho amemhusisha mwanamuziki mkongwe TID.
Wimbo huo ni wa kimahaba ambapo Gigy amekiri kwamba amenasa mpenzi ambaye anatizamia kudumu naye milele. Katika ubeti wake TID anaimba, “Umenijaza nimejaa kwa mtego wako, sasa mimi nina furaha Baby”.
Kwenye chapisho la kutangaza kazi hiyo ya sanaa, Gigy alimmiminia sifa TID kwa kukubali kufanya naye kazi na kwa kuwa mwelekezi wake maishani.
“Hii ni spesheli kwa sababu yako TID. Nyota yako ndio yangu kweli kaka naamini nyimbo yako sasa kwa sababu sisi wote ni Gemini” aliandika Gigy kwenye Instagram, chini ya picha zao za pamoja.
Aliendelea kumshukuru Mungu kwa kumpa maisha marefu TID huku akimwombea aendelee kuwa na maisha hayo marefu kwani yeye ni mtu mzuri.
Huku akimrejelea kuwa shujaa, Gigy alimshukuru TID kwa kumkubali na mapungufu yake na kuendelea kumpa ushauri kila anapokosa wa kumshauri.
“Wewe ni mkubwa sana wazungu wanaita ‘LEGEND’ lakini ninachojua mimi kwangu wewe ni ndugu ni kaka na baba kwa sababu sina baba.” aliendelea kumsifia TID.
Video ya kibao ‘Nimenasa’ imechapishwa kwenye akaunti ya YouTube ya Gigy Money.