Waasi wa Houthi wadai kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani

Waasi hao wanadai kwamba walishambulia ndege za Marekani kwenye meli ya USS Harry S Truman kwa mizinga 18 na droni.

Marion Bosire
2 Min Read

Kundi la waasi wa Houthi nchini Yemen limesema kwamba limelipiza kisasi baada ya kuahidi kujibu mashambulizi makali kwa mashambulizi makali.

Haya yanajiri kufuatia mashambulizi ya angani ya Marekani dhidi ya kundi hilo, yaliyosababisha vifo vya watu 53, Jumamosi.

Msemaji wa wizara ya afya ya Yemen inayoendeshwa na waasi hao wa Houthi, alithibitisha kuongezeka kwa idadi ya vifo hivyo hadi 53 Jumapili.

Watoto watano na wanawake wawili ni kati ya waliofariki kwenye mashambulizi hayo huku kukiwa na majeruhi wapatao 98, kulingana na msemaji huyo Anees Alsbahi.

Msemaji wa jeshi la Houthi Yahya Saree alisema Jumapili kwamba wao ndio walilenga ndege za Marekani kwenye meli ya USS Harry S Truman kwa mizinga 18 na droni.

Marekani haijajibu madai hayo ya Houthi huku Saree akiongeza kwamba Marekani ilikuwa imetekeleza mashambulizi 47 katika maeneo mbali mbali ya Yemen.

Katika maoni tofauti, kiongozi wa kundi la Houthi Abdul Malik al Houthi, alisema kupitia ujumbe kwenye runinga kwamba Marekani na Israel zinataka kulazimisha mipango yao juu ya watu wa eneo hilo.

Alisema watamjibu adui ambaye ni Marekani kwa mizinga na kulenga meli zake za kivita akiongeza kwamba wametishia uchukuzi wa baharini wa Israel kama njia ya kuishinikiza kukubalia misaada ya kibinadamu kuingizwa Gaza.

Afisi ya kisiasa ya Houthi ilitaja mashambulizi ya Marekani kuwa uhalifu wa kivita.

Al-Asbahi alisema kwamba mashambulizi ya Jumamosi yalilenga jiji kuu Sanaa na maeneo ya Saada, Al Bayda na Radaa.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema atatumia nguvu nyingi hadi pale ambapo waasi wa Houthi watakomesha mashambulizi dhidi ya meli za Israel katika bahari ya shamu.

Share This Article