Cocoa Tea afariki

Mwanamuziki huyo ameugua saratani ya limfu kwa muda lakini anaripotiwa kuvamiwa na nimonia kabla ya kifo chake.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki nguli wa mtindo wa reggae Cocoa Tea, amefariki akiwa na umri wa miaka 65.

Malvia Scott mke wa mwanamuziki huyo alithibitisha kifo chake kilichotokea huko Broward, Fort Lauderdale, Florida nchini Marekani Jumanne Machi 11, 2025.

Mke huyo wa Cocoa Tea alielezea kwa,na alipokea simu iliyomfahamisha kwamba mumewe alikuwa amekimbizwa hospitalini kutoka kwa makazi ya uangalizi kwa sababu alikuwa anatapika.

“Alipatikana kuwa na ugonjwa wa lymphoma mwaka 2019, lakini kwa miezi sita iliyopita amekuwa akikabiliwa pia na nimonia.” alielezea Malvia.

Cocoa Tea anaripotiwa kusalia jasiri na mwenye matumaini maishani hata baada ya kupatikana na ugonjwa wa lymphoma kulingana na mkewe.

Ugonjwa wa lymphoma ni aina ya saratani na unahusu ukuaji kupita kiasi wa seli nyeupe za damu ambazo hujaa kwenye mfumo wa limfu ambao ni muhimu kwa kinga ya mwili.

Alipolazwa hospitalini alimtia mkewe moyo kwamba angepona lakini hilo halikutimia.

Cocoa Tea ambaye jina lake halisi ni Calvin Scott alizaliwa mwaka 1959 huko Rocky Point, Clarendon, nchini Jamaica na kwa miaka kadhaa amekuwa nguzo muhimu katika muziki wa reggae.

Wimbo wake wa kwanza uitwao “Searching In The Hill” ulizinduliwa mwaka 1985 akiwa kijana mdogo.Miaka ya 1980 ndiyo alipata kujulikana nchini Jamaica, kabla ya kuwa nyota wa ulimwengi miaka ya 90.

Cocoa Tea ameacha mke kwa jina Malvia na watoto wanane.

Share This Article