Jamaa ajichoma moto nje ya mahakama ya upeo Nairobi

Kulingana na idara ya mahakama jamaa huyo hajatambuliwa na kilichomsukuma ajichome hakijabainika.

Marion Bosire
2 Min Read

Jamaa mmoja ambaye hajatambuliwa vizuri alijichoma moto nje ya mahakama ya upeo katikati mwa jiji la Nairobi leo asubuhi zaa tatu unusu asubuhi.

Kulingana na walioshuhudia tukio hilo, jamaa huyo alikuwa akitembea kwenye barabara ya City Hall akiwa amebeba chupa iliyokuwa na kioevu na stakabadhi fulani kabla ya kusimama kwenye lango la mahakama hiyo.

Akiwa hapo, aliweka stakabadhi hizo chini, akajimiminia kilichokuwa kwenye chupa kinachoaminika kuwa petroli kisha akajiwasha moto.

Walinzi kwenye lango hilo walichukua hatua za haraka wakafika alikokuwa na kumwokoa kwa kuzima moto huo lakini alibaki na majeraha.

Afisa wa polisi anayesimamia masuala ya ulinzi katika mahakama ya upeo, aliwasiliana na kituo cha polisi cha KICC akatumiwa maafisa kadhaa wa polisi hadi eneo la tukio.

Maafisa hao waliwasiliana na serikali ya kaunti ya Nairobi ambayo ilitoa ambulensi ikampeleka jamaa huyo katika hospitali kuu ya Kenyatta.

Polisi hao walichukua pia stakabadhi hizo na nguo zilizokuwa zimechomeka.

Kulingana na taarifa ya msemaji wa idara ya mahakama Paul Ndemo, maafisa wa polisi wanasubiri jamaa huyo atibiwe na hali yake ikiimarika watamhoji ili kumfahamu na kufahamu kilichomsukuma ajichome.

Ndemo amefafanua pia kwamba idara ya mahakama inafuatilia kwa karibu jambo hili ili kufahamu iwapo hatua aliyochukua mtu huyo inahusiana na suala lililoko mahakamani.

Share This Article