Wendy Williams achukuliwa na Ambulensi

Aliandika ujumbe wa kuomba usaidizi kwenye kijikaratasi na kisha kukitupa kupitia dirishani.

Marion Bosire
1 Min Read

Mtangazaji wa zamani wa runinga nchini Marekani Wendy Williams anaripotiwa kuchukuliwa na Ambulensi kutoka kwenye makazi ya kusaidiwa anakoishi. 

Hii ni baada ya kutupa kijikaratasi chenye ujumbe wa kuomba usaidizi kupitia dirishani ambapo maafisa wa polisi walipigiwa simu na waliopata kijikaratasi hicho na wakafika kumjulia hali.

Wendy alipatikana kuwa na ugonjwa wa akili wa dementia miaka minne iliyopita  na amekuwa akiishi kwenye makazi hayo huku akijaribu kukomesha usimamizi aliowekewa kwa lazima na mahakama.

Punde baada ya kutupa kijikaratasi hicho, alionekana akipungia watu mkono dirishani huku akizungumza kwenye simu. Baadaye polisi na wahudumu wa afya walionekana wakimzindikisha na kumbeba kwenye Ambulensi.

Daktari wa akili katika hospitali ya New York alikopelekwa anasema yuko sawa kabisa kwani katika uchunguzi aliofanyiwa alipata alama 10 juu ya 10.

Majibu ya uchunguzi huo yanatarajiwa kuwasilishwa kwa jaji anayeshughulikia kesi ya Wendy ya kutaka kuondolewa chini ya usimamizi.

Haya yanajiri muda mfupi baada ya ripoti kuibuka kwamba Williams anapangiwa kurejea kwenye runinga kwa mara ya kwanza tangu alipoanza kuugua miaka minne iliyopita.

Anapangiwa kuhojiwa kwenye kipindi cha The View cha runinga ya ABC.

Share This Article