Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen amewapongeza washirika wa msaada wa kibinadamu kwa kuendelea kutoa msaada wakati kukiwa na sera zinazobadilika za ufadhili kutoka kwa watoa misaada.
Murkomen amesema msaada huo unasalia muhimu katika kuiondolea nchi hii mzigo inaobeba kwa kuwa mwenyeji wa wakimbizi kutoka nchi mbalimbali waliotafuta hifadhi humu nchini.
Kenya kwa sasa ina wakimbizi zaidi ya 800,000 na kulikuwa na hofu kwamba hatua ya utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani kuondoa ufadhili wa kibinadamu ingeathiri kwa kiwango kikubwa huduma kwa wakimbizi.
Hata hicyo, Waziri Murkomen ameipongeza Marekani kwa kuondoa marufuku dhidi ya ufadhili wa binadamu.
Aliyasema hayo wakati wa mkutano wa ushauriano na mabalozi, makamishna wakuu na wakuu wa taasisi za kifedha uliofanyika katika hoteli moja jijini Nairobi leo Jumatatu na kuangazia hali ya wakimbizi humu nchini.
Kwa upande wao, Mabalozi hao na washirika wengine walipongeza Mpango wa Shirika unaoendeshwa na serikali unaolenga kuwashirikisha wakimbizi katika shughuli za kiuchumi za kila siku humu nchini. Wamesema mpango huo siyo tu kwamba utakuwa wenye manufaa kwa wakimbizi bali pia kwa jamii wenyeji na kwa nchi kwa jumla.
Ushiriki wa umma na uboreshaji wa mpangokazi huo wa udhibiti, ambao ni muhimu kwa mafanikio ya Mpango wa Shirika, unaendelea.
Washirika wa maendeleo wanaunga mkono mpango huo na wanafanya kazi bega kwa bega na nchi wenyeji ili kuhakikisha uzinduzi wake unafanikiwa.