Rita Edochie awatupia wahubiri swali

Alitaka kujua watakachofanya ili kujimudu iwapo watu watakoma kwenda kanisani.

Marion Bosire
1 Min Read
Rita Edochie

Mwigizaji wa muda mrefu wa filamu za Nigeria almaarufu Nollywood Rita Edochie amewarushia wahubiri swali gumu.

Kupitia akaunti yake ya Instagram Rita aliwauliza, “Wahubiri iwapo watu watakoma kabisa kwenda kanisani katika muda wa miaka miwili ijayo, kazi yenu itakuwa gani?”

Mama huyo ambaye ni shemeji ya mwigizaji mwenza Pete Edochie aliendelea kusema kwamba anauliza swali hilo kwa sababu kwa mtazamo wake, falme zinagawanyika katika ukristo, uasilia na hata dini nyingine.

“Mambo yanabadilika haraka na imani ya watu na mitindo yao ya maisha pia inabadilika. Leo dini na uhusiano wa watu na Mungu wao unabadilika.” aliendelea kusema.

Rita alimulika wahubiri ambao alisema hawana namna nyingine ya kujipatia kipato isipokuwa sadaka inayokusanywa katika maeneo ya ibada na mabadiliko yakija itakuwa vigumu kwao kujimudu.

Kulingana naye, hata ingawa wengi wa wahubiri huchukulia kazi yao kuwa wito wa pekee kutoka kwa Mungu, hilo haliwazuii kutafuta namna nyingine ya kujipatia mapato.

“Wajifunze kutokana na haya.” alimalizia mama huyo huku akiwatakia wafuasi wake Jumapili njema.

Share This Article