Vinka akaribisha wazo la kufungua kampuni yake ya muziki

Aliyasema hayo kwenye mahojiano alikosisitiza kwamba hata ingawa ataanzisha kampuni ataendelea kuwa chini ya usimamizi wa Swangz Avenue.

Marion Bosire
2 Min Read

Msanii wa muziki nchini Uganda Veronica Nakiyingi maarufu kama Vinka amesema kwamba yuko wazi kwa wazo la kuanzisha kampuni yake ya kurekodi muziki na kusimamia wanamuziki.

Vinka ambaye amesajiliwa na kampuni ya Swangz Avenue, alifichua hilo alipokuwa akijibu maswali kuhusu uvumi unaosambaa kuhusu kandarasi za wasanii wenzake katika kampuni ya Swangz.

Alifafanua kwamba hata ingawa anapata wazo la kuanzisha kamouni yake, haondoki Swangz Avenue hivi karibuni, kwani hahisi kama anaweza kujisimamia kama msanii.

Msanii huyo anasema katika maisha yake yote amekuwa mtu wa mpangilio na hivyo hawezi kuwa bila usimamizi. “Ninawezaje kuishi maisha ambapo simu zote napokea mimi?” alishangaa Vinka.

Aliwataka wasanii waelewe kwamba kuna watu lazima pia wanufaike na pesa ambazo wanalipwa kwani ni biashara. “Iwapo unafanya kazi na mtu ni lazima achukue asilimia fulani ya malipo yako.” alisema.

Jambo lingine ambalo msanii huyo alifichua ni kwamba katika uhalisia yeye ni mtu mwenye aibu sana na kwa sababu yeye ni msanii analazimika kuishi maisha mara mbili, kama yeye na kama msanii.

Wakati wa kuwa msanii, Vinka alisema anakuwa mwazi na anayependa watu lakini wakati hayupo jukwaani na anaendeleza maisha kama Veronica, yeye huwa mwoga sana.

Hali hiyo huchukuliwa na wengi kimakosa kuwa kiburi huku akihimiza mashabiki kuelewa kwamba Vinka ni mwazi na mpenda watu lakini Veronica ni mwoga na mwenye aibu.

Share This Article