Serikali ya muda ya Syria imetuma wanajeshi zaidi kwenye miji yake ya Pwani katika eneo la Kaskazini Magharibi ambapo wanajeshi wamekuwa wakikabiliana na wapiganaji waaminifu kwa kiongozi wa awali Bashar al-Assad.
Vurugu hizo ambazo zinaripotiwa kusababisha vifo vya wengi wakiwemo raia, ndizo changamoto kubwa iliyokabili serikali hiyo mpya iliyochukua mamlaka Disemba 2024 kufuatia kubanduliwa kwa al-Assad.
Wanajeshi walikuwa wameripoti awali kwamba wametwaa udhibiti wa maeneo kadhaa ya majimbo ya Tartous na Latakia ambapo wapiganaji waaminifu kwa Assad walikuwa wametekeleza mashambulizi Alhamisi.
Shirika la habari la serikali ya Syria SANA lilinukuu afisa mmoja wa usalama aliyesema kwamba baada ya mashambulizi, watu wengi walikwenda kwenye miji ya Pwani kulipiza kisasi mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa serikali.
Afisa huyo alisema hatua hiyo ilisababisha ukiukaji wa watu kadhaa suala ambalo wanashughulikia kwa nia ya kulitokomeza.
Sheria ya kutotoka nje usiku bado inatekelezwa huko Latakia na katika maeneo mengine ya Pwani ambayo yanakaliwa na wafuasi wa Al-Assad wa kundi la Alawite, na wamekuwa wakimuunga mkono kwa muda mrefu.
Katika usemi wake wa kwanza hadharani tangu vurugu kuzuka, Rais wa muda wa Syria Ahmed al-Sharaa Ijumaa aliwataka wapiganaji hao kuachilia silaha na kujisalimisha kabla muda haujakwisha.
Al-Sharaa, kamanda wa wapiganaji wa upinzani waliomwondoa al-Assad mamlakani baada ya miaka 14 ya vita, alisema serikali itawatafuta wafuasi sugu wa serikali iliyoanguka na kuwafikisha kwenye mahakama ya haki.