Verydarkman asema hataweza kulipa Mercy Chinwo

Chinwo alimshtaki kwa kuingilia ugomvi wake na meneja wake wa zamani, akidai fidia.

Marion Bosire
2 Min Read

Mkosoaji wa mitandaoni nchini Nigeria Verydarkman – VDM ambaye jina lake halisi ni Martins Vincent Otse amejitetea kutokana na kesi ambayo mwimbaji Mercy Chinwo aliwasilisha dhidi yake.

Katika video aliyochapisha mitandaoni VDM alielezea kwamba hana uwezo wa kutoa fidia ya Naira Bilioni 1.1 anayodaiwa na Chinwo kwani anakabiliwa na kesi kadhaa za kuharibia watu sifa na wanadai fidia.

Chinwo aliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya VDM baada yake kutoa maoni yake kuhusu kisa kinachoendelea cha Chinwo kuzozana na meneja wake wa zamani.

Kulingana na stakabadhi za mahakama, Chinwo kupitia kwa wakili wake Pelumi Olajengbesi, aliwasilisha kesi hiyo katika mahakama kuu ya Abuja Machi 3, 2025.

Anayotaka ni VDM aombe msamaha hadharani kwa maneno aliyoyasema kumhusu, afute video au machapisho yoyote ya usemi huo na ajitokeze mahakamani katika muda wa siku 14, kando na kumfidia.

VDM anasema ameshtakiwa na watu kadhaa ambao wanamtaka awalipe fidia na iwapo watamshinda kwenye kesi hizo basi hataweza kuwalipa huku akichagua kuomba msamaha.

“Mwili wa Kristo umeshtaki. Mercy Chinwo, nisamehe. Mimi sina hela. Hata pesa za NGO sio nyingi hivyo. Ninajua siwezi kuendelea na hii kesi. Ni bora niombe msamaha. Mercy usikubali kutumiwa na shetani.” alisema Verydarkman.

Chinwo ambaye ni mwimbaji wa nyimbo za injili hajajibu ombi hilo la msamaha.

Share This Article