Washukiwa wa uhalifu wanaswa Kisii

Wawili hao wanaoaminika kutekeleza visa vya uhalifu katika eneo hilo, walipatikana wakiwa na bunduki.

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa upelelezi wa jinai wamekamata washukiwa wawili wa uhalifu katika eneo la Daraja Mbili kaunti ya Kisii baada ya kupashwa habari.

Wawili hao wanaoaminika kutekeleza visa vya uhalifu katika eneo hilo, walipatikana wakiwa na bunduki.

Gerald Nyambarika Okumu na James Ochieng, ambao wote wana umri wa miaka 35, walikamatwa wakiwa kwenye pikipiki aina ya Blue TV Star nambari ya usajili KMEK 866M, katika kituo cha petroli cha Texas, tayari kutekeleza mipango yao.

Msako mkali waliofanyiwa uliishia katika kupatikana kwa bunduki aina ya Bernardelli 60, iliyokuwa na risasi tano ndani ambayo ilikuwa imefichwa na James Ochieng aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo.

Gerald Nyambarika Okumu naye alipatikana akiwa amebeba vyuma vinne vilivyoundwa kwa njia ambayo vinaweza kufyatua na simu nne za rununu, ishara kwamba walikuwa tayari kutekeleza uhalifu.

Kwa sasa washukiwa hao wanazuiliwa na maafisa wa polisi huku wapelelezi wakiendeleza uchunguzi kubaini visa vya uhalifu wanavyohusishwa navyo katika eneo hilo.

Vitu ambavyo walipatikana navyo; bunduki, vyuma na simu za rununu vinashikiliwa na polisi pia kama ithibati.

Share This Article