EACC imetwaa shilingi milioni 12.8 kutoka kwa mshauri wa zamani wa kaunti ya Taita Taveta

Tom Mathinji
1 Min Read
Makao Makuu ya EACC Jijini Nairobi.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi hapa nchini EACC, imetwaa shilingi milioni 12.8 kutoka Geoffrey Kimonge, msaidizi wa zamani wa aliyekuwa Gavana wa Taita Taveta John Mruttu.

Hatua hiyo ilitokana na uamuzi wa mahakama iliyompata na hatia ya kupata mali ya umma kupitia njia za ulaghai.

Katika uamuzi uliotoleewa Februari 28, 2025, Hakimu Mkuu wa Voi Mildred Obura, alisema Kimonge alipata fedha kinyume cha sheria kwa kupokea malipo za shughuli ambazo hazikutekelezwa akiwa mshauri wa serikali ya kaunti hiyo.

Mahakama hiyo ilimwagiza Kimonge kulipa serikali shilingi milioni 12,458,990, pamoja na riba kuanzia siku alipokea fedha hizo hadi wakati wa kukamilisha malipo.

Tume ya EACC ilianzisha uchunguzi mwaka 2020, baada ya kupokean malalamishi kwamba Kimonge amepokea shilingi Milioni 13.8 kama malipo, zilizodaiwa kuwa marupurupu ya wawakilishi wadi na wafanyakazi wa kaunti.

“Ilidaiwa kuwa mshauri huyo wa zamani wa kisiasa, alipokea shilingi 13,878,587 zilizodaiwa kuwa marupurupu ya wawakilishi wadi na wafanyakazi wa serikali ya kaunti hiyo,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamoud kupitia kwa taarifa.

Share This Article