Viongozi wa upinzani wamekutana leo Jumanne kwa kusudi la kupanga mikakati ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa chama kipya cha PLP Martha Karua.
Wengine waliohudhuria ni kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa, Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Onyonka na kiongozi wa chama cha Safina Jimi Wanjigi.
Awali, viongozi hao waliashiria kuwa watatangaza muungano mpya wa kisiasa utakaomenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Viongozi hao wanakutana wakati ambapo kinara wa chama cha ODM Raila Odinga anatarajiwa kutangaza mwelekeo wake wa kisiasa wakati wowote kuanzia sasa.
Raila anasema kwa sasa anakusanya maoni ya Wakenya na tayari amezuru maeneo ya Busia, Mombasa na Kilifi.
Chama cha ODM tayari kimepatiana baadhi ya wanachama wake kuwa Mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho cha chungwa wanamshinikiza Raila kutangaza rasmi kuungana na utawala wa Kenya Kwanza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.