Shirika la Global Fund limetafuta usaidizi wa Rais William Ruto kukusanya fedha za kukabiliana na Virusi vya Ukimwi (VVU), kifua kikuu na malaria.
Shirika hilo limemtaka Rais Ruto kutumia mitandao yake duniani kusaidia kuchangisha fedha hizo.
Global Fund imetoa wito huo kwa kiongozi wa nchi kupitia barua iliyomwandikia Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi.
Kwenye barua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Peter Sands amemtaka Rais Ruto kulisaidia wakati wa Ushehenezaji Tena wa Nane.
Kulingana na barua hiyo, ombi hilo linakuja wakati muhimu ambapo ufadhili wa nje wa sekta ya afya unakabiliwa na tishio kubwa.
“Kutokana na dhamira na uongozi wako Rais Ruto, nina imani unaweza ukatimiza Ushehenezaji Tena wa Nane wenye mafanikio,” alisema Sands kwenye barua yake.
“Hii itawezesha Global Fund kuendelea kuisaidia Kenya na nchi zingine kote barani Afrika kuokoa maisha.”
Sands aliongeza kuwa kutokana na changamoto zinazoshuhudiwa duniani kwa sasa, kuna umuhimu zaidi wa kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha hatua endelevu zinafikiwa katika kukabiliana VVU, kifua kikuu na malaria na katika kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.
Kenya na Global Fund zimekuza ushirikiano thabiti huku shirika hilo likiwekeza zaidi ya shilingi bilioni 300 nchini humo.
Wito wa shirika hilo unakuja wakati Marekani imetangaza kusitishwa kwa ufadhili unaotolewa kwa mataifa mbalimbali hususan yanayostawi katika kukabiliana na maradhi hayo duniani.
Ufadhili huo ulisitishwa baada ya Rais Donald Trump kuingia madarakani Januari 20 mwaka huu.
Nchi nyingi zilizoathiriwa sasa zimeazimia ktafuta ufadhili mbadala wakati kukiwa na hofu kwamba hatua ya Marekani huenda ikawa pigo kwa juhudi zilizoafikiwa katika kukabiliana na magonjwa hayo.