Serikali yasema Wakenya 64 bado wamekwama Myanmar

Martin Mwanje
1 Min Read
Musalia Mudavadi - Waziri wa Mambo ya Nje

Wakenya 64 bado wamekwama nchini Myanmar, wakisubiri kuvuka mpaka kuelekea nchini jirani ya Thailand. 

Wizara ya Mambo ya Nje kwenye taarifa inasema Wakenya hao wanasubiri kwenye mpaka uliopo kati ya Thailand na Myanmar.

Hii ni baada ya kuokolewa kutoka kwenye vituo vya ulaghai nchini Myanmar.

“Balozi wa Kenya nchini Thailand ameendelea kuwasiliana na Wakenya hao kila siku ili kuwajuza juhudi zinazofanywa na serikali kuwarejesha nyumbani salama,” ilisema Wizara ya Mambo ya Nje kwenye taarifa hiyo.

Wakenya hao 64 ni sehemu ya kundi la zaidi ya raia wa kigeni 7,000 waliookolewa kutoka kwenye vituo vya ulaghai na makundi mawili yenye silaha ambayo ni DKBA na lile la Kikosi cha Ulinzi wa Mpaka  (BGF).

Raia hao wa kigeni hawajavuka mpaka kuelekea Thailand kwa sababu mamlaka za nchi hiyo hazijafungua kivuko kilicho kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili tangu Februari 12 mwaka huu.

Huo ni wakati ambapo kundi la kwanza la raia 260 wa kigeni, wakiwemo Wakenya 23, walikabidhiwa kwa Jeshi la Kifalme la Thai na Jeshi la Kibuddha la Demokrasia la Karen  (DKBA).

 

Share This Article