Mgonjwa wa pili wa Ebola, mtoto mwenye umri wa miaka minne, amefariki nchini Uganda, limesema Shirika la Afya Duniani (WHO), likiinukuu Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
Kifo hicho kinafikisha 10 idadi ya visa vilivyothibitishwa nchini Uganda.
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilitangaza kuzuka kwa ugonjwa huo mwezi Januari baada ya kifo cha muuguzi mwanamume katika Hospitali ya Rufaa ya Mulago katika mji mkuu Kampala.
Ofisi ya WHO ya Uganda ilichapisha taarifa usiku wa Jumamosi, kwamba Wizara ya Afya ya Uganda iliripoti kisa kingine cha Ebola katika hospitali ya Mulago cha mtoto wa umri wa miaka minne na nusu, ambaye aliaga dunia siku ya Jumanne.
Mulago ndiyo hospitali pekee ya kitaifa ya rufaa kwa wagonjwa wa Ebola.
Wizara hiyo imesema Februari 18, wagonjwa wote wanane wa Ebola waliokuwa chini ya uangalizi wameruhusiwa lakini watu wasiopungua 265 wamesalia chini ya karantini kali jijini Kampala na miji mingine miwili.
Dalili za Ebola ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa na misuli. Virusi hivi huambukizwa kwa kugusana na majimaji ya mwili wa mtu mwenye maambukizo.