Tanzania kujenga ukumbi wa matamasha

Msemaji wa serikali ya Tanzania alisema ujenzi huo utaanza punde baada ya fedha za kuufadhili kupokelewa.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali ya Tanzania ina mipango ya kujenga eneo maalum kwa ajili ya maandalizi ya matamasha na maonyesho mbali mbali ya sanaa.

Haya ni kulingana na msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania gerson Msigwa.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jana, Msigwa alisema, “Arena inakuja, Wasanii mumshukuru sana Rais Samia, tumekuwa na mipango ya muda mrefu kuhusu mradi huu lakini hatimaye Rais amepata fedha.”

Aliongeza kusema kwamba fedha hizo ni sehemu ya mkopo wa masharti nafuu, na zitatumiwa kwa ujenzi wa ukumbi huo maalum na Kijiji cha Filamu.

Msigwa aidha alisisitiza kwamba ujenzi wa maeneo hayo muhimu ya sanaa utaanza punde baada ya pesa hizo kutolewa.

Msigwa alikuwa anajibu wito uliotolewa na msanii wa muziki Diamond Platnumz usiku wa tuzo za Trace katika kisiwa cha Zanzibar, kutokana na changamoto zilizoshuhudiwa.

Usiku huo wa Februari 26, 2025, upepo mkali kutoka baharini ulisababisha matatizo kwenye tamasha hilo ambalo lilianza kwa kuchelewa.

Lilipoanza baada ya saa nne usiku, hitilafu ya mitambo ikasababisha kukatizwa kwa matangazo ya moja kwa moja. Waandalizi hata hivyo waliahidi kuchapisha video za tamasha hilo wiki ijayo.

Share This Article