Rais Ruto ahimiza umoja kati ya viongozi

Rais alikuwa akizungumza katika mazishi ya Seneta William Cheptumo.

Marion Bosire
2 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto kwa mara nyingine, amehimiza umoja kati ya viongozi wote wa Kenya, wale wa upande wa serikali na hata wale wa upinzani.

Kiongozi wa nchi alikuwa akizungumza hayo jana alipoongoza taifa katika mazishi ya Seneta wa Baringo William Cheptumo, katika uwanja wa shule ya upili ya Arap Moi, ambapo hafla hiyo iliandaliwa.

Katika hotuba yake, Rais alimwomboleza Cheptumo akimtaja kuwa muungwana, mwanasiasa aliyekuwa na maono na kiongozi mwenye shauku.

Aliendelea kwa kumpongeza marehemu Cheptumo kwa kusimama kidete na nchi yake kila alipohitajika kufanya hivyo, akitaja jukumu lake kubwa katika utatuzi wa mgogoro wa uchaguzi wa mwaka 2007.

Kulingana na Rais Ruto, sauti yenye nguvu ya Cheptumo ilizungumza kwa niaba ya wasiokuwa na sauti kwa njia ya uaminifu, na hivyo kuendeleza amani na utulivu huko Baringo na katika bonde la Kerio.

Rais Ruto alilalama kwamba kifo cha Cheptumo kimekomesha maisha ya kipekee na taaluma ya kuvutia ya kisiasa, alama ya kudumu katika historia ya mabadiliko ya nchi.

Marehemu Seneta wa kaunti ya Baringo William Cheptumo alizikwa jana nyumbani kwake katika kijiji cha Tunoiywo, Bartabwa, kaunti ya Baringo.

Aliaga dunia Februari 15, 2025, akiwa na umri wa miaka 57 wakati akiendelea kupokea matibabu katika hospitali moja ya Nairobi.

Share This Article