Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga sasa anasema ataamua hatima yake ya kisiasa baada ya kusikiliza maoni ya watu.
Raila ameripotiwa akisema atatoa tangazo la mwelekeo wake wa kisiasa wiki ijayo.
“Sasa tumesema siku ya leo tukisherehekea, Baba amerudi na nimesema nitakuja kuuliza watu wangu wote kwanza mwelekeo,” alisema Raila leo Ijumaa mjini Busia wakati wa maadhimisho ya miaka 20 tangu kuasisiwa kwa chama cha ODM.
“Sisi si watu wa kufuata watu ovyoovyo. Tunafuata watu na sababu. Chama cha ODM ni chama ambacho kina sera kamili na msimamo. Na vilevile sisi tumekuwa tukitetea haki ya wananchi wa Kenya na tutaendelea kutetea haki ya wananchi wa Kenya.”
Matamshi ya Raila yanakuja wiki mbili baada ya kubwagwa katika juhudi zake za kutaka kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Punde baada ya kurejea nchini baada ya kulambishwa sakafu jijini Addis Ababa, Raila alielekea moja kwa moja katika eneo la Pwani alikokutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Mombasa.
Uvumi umekuwa ukienea kwamba Raila anadhamiria kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Hususan, chanzo cha uvumi huo ni hatua ya chama cha chungwa kuridhia baadhi ya wanachama wake kuteuliwa kama Mawaziri katika serikali ya Kenya Kwanza.
Wao ni John Mbadi (Waziri wa Fedha), Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika) na Hassan Ali Joho (Waziri wa Madini), mawaziri ambao wamekuwa wafuasi sugu wa utawala wa sasa.
Kwa upande mwingine, upinzani unaonekana kummezea mate Raila wakati ukijipanga kukabiliana na Rais Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.
Umemtaka Raila kutangaza peupe msimamo wake wa kisiasa haraka iwezekanavyo ili mipango ya kuelekea uchaguzi huo ianze kukarabatiwa asubuhi na mapema.