PLP ni chama cha matapeli, hakina sera, asema Rais Ruto

Chama cha PLP (zamani kikijulikana kama Narc Kenya) kilizinduliwa jana Alhamisi katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa upinzani. Kiongozi wa PLP ni Martha Karua.

Martin Mwanje
2 Min Read
Viongozi wa upinzani wakati wa uzinduzi wa chama cha PLP

Rais William Ruto amepuuzilia mbali chama kipya cha People’s Liberation Party (PLP) kilichozinduliwa jana Alhamisi. 

Uzinduzi wa chama hicho cha Martha Karua ulihudhuriwa na Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka miongoni mwa viongozi wengine wa upinzani.

Awali, viongozi hao waliashiria kuwa wataunda muungano wa kisiasa utakaotoana jasho na ule wa Kenya Kwanza wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Wakati wa uzinduzi wa jana Alhamisi, viongozi hao wa upinzani walitumia fursa hiyo kuishtumu serikali ya Rais William Ruto kwa kuwa chanzo cha masaibu yanayowakumba Wakenya.

Wakijinadi kama wakombozi na watetezi nambari moja wa Wakenya, waliahidi kukabiliana na masaibu yanayowakumba Wakenya kwa sasa ikiwa ni pamoja na gharama ya juu ya maisha punde watakapomtema Rais Ruto kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Hata hivyo, saa chache baada ya uzinduzi wa chama cha PLP kinachochukua mahali pa Narc K, Rais Ruto amekipuuzilia mbali chama hicho cha rangi ya zambarau.

“Wengine naona wanajaribu kukutana sijui wanafanya mkutano, ati wanatengeneza chama. Ile chama wanajaribu kutengeneza, wanaongea massaa manne juu ya William Ruto. Masaa manne? Sasa mimi nauliza nyinyi, kwani hii chama walikuwa wanatengeneza ilikuwa ya William Ruto? Ama hiyo chama inaitwa William Ruto?” alishangaa kiongozi wa nchi wakati akiendelea na ziara yake katika eneo la Pwani.

“Sasa nyinyi, sera yenu, William Ruto, mpango wenu, William Ruto, maono yenu, William Ruto. Sasa mimi nataka niwaambia wale jamaa na niwatangazie Wakenya, hawa watu ambao walikuwa wanaongea mambo ya William Ruto, mimi sijawatuma. Hiyo chama wanaongelea hapo siyo ya William Ruto. Kwa hivyo, hawa ni matapeli.”

Hayo yanajiri wakati ambapo Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini (COTU) Francis Atwoli ameahidi kuwa hatakishtaki chama cha PLP kwa kutumia rangi yake ya zambarau.

Katika kuchukua hatua hiyo, Atwoli anasema COTU ni muungano mkubwa zaidi unaotambuliwa kimataifa na hauwezi ukafungua ukurasa mpya wa mizozo na vyama vidogo vya kisiasa vinavyotambuliwa tu humu nchini.

Atwoli amebashiri kuwa chama cha PLP kitakumbana na mauti ya kisiasa hivi karibuni.

 

 

Share This Article