Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, amesema ameshiriki mashauriano na balozi wa Japani hapa nchini Hiroshi Matsuura, kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Japani.
Kupitia ukurasa wa X, Mudavadi alisema hayo yaliangazia kuboresha sekta za biashara, uwekezaji, teknolojia na elimu.
“Japan inasalia kuwa mshirika wa kuaminika na wa dhamana, na tumejitolea kuimarisha ushirikiano huu wa miongo sita ambao nguzo zake ni kuaminiana na heshima,” alisema Mudavadi.
Kulingana na waziri huyo wa Mambo ya Nje, mazungumzo hayo pia ayalilenga kutambua mikakati itakayoleta mabadiliko yatakayowafaidi wananchi wa mataifa hayo mawili.

“Pamoja tutashughulikia changamoto za pamoja na kutafuta fursa mpya za kiuchumi, kupanua sekta za utengenezaji bidhaa, kilimo, afya,mabadiliko ya kidijitali na miundo mbinu,” aliongeza Mudavadi.
Aliyasema hayo wakati wa sherehe ya 65 ya kuzaliwa kwa mfalme Naruhito , ambaye ni mfalme wa 126 wa Janapi, iliyoandaliwa katika makao rasmi ya balozi wa Japan hapa nchini.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na raia wa Japani hapa nchini pamoja na marafiki wa Japani hapa nchini Kenya.