Rais Ruto: Serikali itahakikisha umeme unasambazwa katika pembe zote za nchi

Tom Mathinji
2 Min Read
Rais Ruto azuru kituo cha usambazaji umeme (KETRACO) cha Mariakani.

Rais William Ruto leo Alhamisi alifanya ziara ya ukaguzi katika kituo cha Mariakani cha kusambaza nguvu za umeme (KETRACO) katika kaunti ya Kilifi.

Mradi huo unalenga kuimarisha usambazaji wa nguvu za umeme kati ya Mombasa na Nairobi na kupiga jeki ukuaji wa kiviwanda hususan katika eneo la Pwani.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa taifa alisema serikali yake imejitolea kuhakikisha umeme unasambazwa katika pembe zote za taifa, ili kuboresha ukuaji wa uchumi wa taifa hili.

“Tunaongeza usambazaji wa nguvu za umeme katika kona zote za taifa hili, kuleta mwangaza katika nyumba zetu, kuchochea ukuaji wa viwanda, kubuni nafasi za ajira na kupiga jeki ukuaji wa uchumi,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto katika kituo cha usambazaji umeme (KETRACO) cha Mariakani, kaunti ya Kilifi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa KETRACO Dkt. Mhandisi. John Mativo, alisema kuwa kituo hicho kitapunguza utumizi wa mafuta ya diseli katika uzalishaji nguvu za umeme ambao ni ghali katika eneo la pwani.

“Kituo hicho kitasambaza umeme kati ya Mombasa na Nairobi kwa kupunguza kupotea kwa umeme wakati wa usafirishaji na hivyo kufanikisha shughuli ya usambazaji umeme,” alisema Dkt. Mativo.

Kituo hicho kinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo Barani Afrika (AfDB)), kupitia mradi wa umeme kati ya Kenya na Ethiopia, unaolenga  kuhakikisha eneo la pwani lina mfumo imara wa usambazaji umeme.

Rais Ruto kwa sasa yuko katika ziara ya maendeleo eneo la Pwani, ambako pia alizindua mradi wa kawi ya miale ya jua (KOSAP)  katika kisiwa cha Ndau kaunti ya Lamu.

 

Share This Article