Rais Ruto aahidi huduma kwa Wakenya wote

Rais Ruto alikuwa akizungumza katika kaunti ya Lamu, anapoendeleza ziara ya kikazi ya eneo la Pwani.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais William Ruto amesisitiza kwamba serikali yake itaendelea kutoa huduma katika sehemu zote za taifa hili, ili kuhakikisha ukuaji jumuishi wa uchumi.

Akizungumza leo wakati akizindua mradi wa umeme unaotokana na miale ya jua katika kisiwa cha Ndau kaunti ya Lamu, Rais alisema hakuna sehemu yoyote ya nchi itaachwa nyuma kimaendeleo kwa sababu za kisiasa na kikabila.

Kiongozi wa nchi alisisitiza kwamba ujumuishaji ni muhimu katika kusongesha nchi mbele, akisema hakuna kundi linafaa kuhisi kwamba limetelekezwa katika utawala.

Alihakikishia Wakenya kwamba serikali imejitolea kuhakikisha ufanisi wa mpango wake wa kiuchumi wa Bottom-Up Economic Transformation Agenda – BETA.

Wakati huo huo, Rais amekashifu wale ambao wanataka kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila na kimaeneo akisema juhudi zao zitaambulia patupu.

Rais Ruto alisema hakuna haja ya kujihusisha na chuki na siasa za kikabila akiongeza kusema kwamba kazi yake ni kuunganisha Wakenya wote.

Kiongozi wa nchi aliwataka Wakenya wawe macho na waepuke viongozi ambao hutumia ukabila kupata uongozi.

Alitoa wito kwa Wakenya wote kusalia na umoja ili waweze kusonga mbele kama nchi moja yenye amani iliyo na maono sawa.

Kiongozi wa nchi vile vile aliwataka watu wa kaunti ya Lamu kuishi pamoja kwa amani bila kuzingatia utofauti wa dini, kabila na miegemeo ya kisiasa.

Share This Article