Bien ashinda tuzo ya Trace Zanzibar

Hafla ya kugawa tuzo za Trace iliandaliwa usiku wa jana huko Zanzibar.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Bien Aime au ukipenda Bien Barasa ndiye mshindi wa tuzo ya msanii bora mashariki mwa Afrika kwenye awamu ya pili ya tuzo za Trace mwaka 2025.

Haya ni kulingana na bango alilochapisha mtangazaji wa Kenya Azeeza Hashim ambaye alihudhuria tuzo hizo huko Zanzibar jana usiku.

Bien alikuwa msanii wa pekee wa Kenya ambaye aliteuliwa kuwania tuzo hizo na aliteuliwa kwenye kitengo hicho pekee, hata ingawa ziliandaliwa Afrika Mashariki.

Alikuwa anashindana na wasanii kama Joshua Baraka wa Uganda, Rophnan wa Ethiopia na wasanii wa Tanzania Diamond Platnumz, Harmonize, Marioo, Zuchu na Nandy.

Kando na uwaniaji, Bien pia alikuwa mmoja wa waliotumbuiza kwenye hafla ya kugawa tuzo za Trace katika hoteli ya kifahari ya Mora.

Amesifiwa sana na wengi waliofuatilia hafla hiyo kutokana na uwezo wake wa kutumbuiza moja kwa moja jukwaani na wala sio kutumia muziki uliorekodiwa.

Wadadisi na wakosoaji wa mitandaoni wanahisi kwamba yeye ni mmoja wa wasanii ambaye aliweza kudhibiti sauti yake jukwaani huku wengine wengi wakishindwa.

Wasanii wengi hasa wa tanzania walikosolewa kwa kuzingatia sana kucheza densi na walikuwa na wacheza densi na hivyo kushindwa kudhibiti sauti zao kutokana na kuhema sana baada ya kucheza.

Share This Article