D’Banj aahidi kutumbuiza kwa harusi ya Jux

Alitoa ahadi hiyo alipokutana na Jux huko Zanzibar ambapo wamejumuika kwa ajili ya tuzo za Trace.

Marion Bosire
1 Min Read
D'Banj

Mwanamuziki wa muda mrefu nchini Nigeria Oladapo Daniel Oyebanjo, maarufu kama D’Banj ameahidi kutumbuiza kwenye harusi inayotarajiwa ya mwanamuziki wa Tanzania Juma Jux nchini Nigeria.

Alitoa ahadi hiyo alipokutana na Jux na Diamond Platnumz huko Zanzibar ambapo wamejumuika kwa ajili ya tuzo za leo za Trace.

Katika video ambayo imesambazwa mitandaoni, D’Banj anasikika akimwambia Jux kwamba jambo ambalo amefanya kwa kuoa Priscilla Ojo kutoka Nigeria ni la heshima na wanapotizama video zao wanaona kwamba wana upendo wa kweli.

“Kitu cha pekee ambacho nitakupa kwa sababu ulichokifanya ni upendo wa dhati nitaimba kwenye harusi yako ijayo. Nitaimba ‘Fall in Love’.” alisema D’Banj.

Diamond ambaye pia alionekana mwenye furaha alisikika akisema, “Tunaoa kutoka nchini kwenu”. Ikumbukwe kwamba Diamond na Zuchu walikuwa na jukumu kubwa katika harusi ya Jux na Priscilla.

Jux ambaye yuko Zanzibar pamoja na mkewe Priscilla tayari wamefunga ndoa nchini Tanzania ambayo ilikuwa na hafla tatu, na sasa hafla mbili zimesalia na zinatarajiwa kuandaliwa nchini Nigeria mwezi Aprili mwaka huu.

Share This Article