Wetang’ula awaongoza wabunge kumwomboleza Chebukati

Mwenyekiti huyo wa zamani wa IEBC alifariki Alhamisi wiki jana akiwa na umri wa miaka 63. Alifariki kutokana na mshtuko wa moyo na alikuwa akiugua saratani ya ubongo.

Martin Mwanje
1 Min Read
Moses Wetang'ula - Spika wa Bunge la Taifa
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula aliwaongoza wabunge katika kutembelea makazi ya Nairobi ya Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati ili kuifariji familia yake. 
Chebukati, aliyekuwa na umri wa miaka 63, alifariki Alhamisi wiki iliyopita katika hospitali moja jijini Nairobi kutokana na mshtuko wa moyo.
Alikuwa akipokea matibabu hospitalini humo baada ya kuugua saratani ya ubongo, ugonjwa aliougua kwa muda mrefu.
Chebukati anakumbukwa kwa kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 na 2022, chaguzi ambazo zilikumbwa na utata hususan kuhusiana na matokeo ya urais.
Kiasi kwamba mnamo mwaka 2017, Mahakama ya Juu iliagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa urais ambao mshindi wake alikuwa ni Rais Uhuru Kenyatta baada ya kususiwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Wakati wa ziara yao nyumbani kwa Chebukati, Spika Wetang’ula aliusifu uongozi wa marehemu, akisisitiza jukumu kubwa alilotekeleza katika kusimamia IEBC.
“Ofisi ambayo Wafula Chebukati alishikilia ilimfanya atambue kwamba utekelezaji wa majukumu yake haukuwa tu wa kimwili; ulikuwa wa kisheria, wenye akili na kikatiba. Na alitekeleza wajibu wake kwa uadilifu hadi mwisho kabisa. Huyo ndiye mtu shupavu tunayejiandaa kumwaga hivi karibuni,” aliungama Wetang’ula.

Chebukati amepangiwa kuzikwa Machi 8 nyumbani kwake huko Kitale, kaunti ya Trans Nzoia.
Share This Article