Papa Francis alilala vizuri usiku wa kuamkia leo Jumatano na anaendelea kupumzika wakati akiendelea kupokea matibabu.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amekuwa akipokea matibabu dhidi ya ugonjwa wa mkamba kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Hii ni baada ya kulazwa katika hospitali ya Gemelli katika jiji la Roma nchini Italia Februari 14, 2025 akiugua ugonjwa huo uliomsababishia matatizo ya kupumua.
“Papa amelala salama usiku na yupo anapumzika,” ilisema taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican leo Jumatano.
Ofisi hiyo jana Jumanne ilitoa maelezo kuhusu hali ya kliniki ya Papa Francis ambayo “imesalia kuwa tete,lakini thabiti”.
Kulingana na ofisi hiyo, hakuna matukio ya kupumua kwa haraka na vigezo vya vipimo vya damu vya Papa Francis vinaendelea kuwa thabiti.
Waumini wa Kanisa Katoliki kote duniani wamekuwa wakimwombea Papa huyo mwenye umri wa miaka 88 kupata nafuu ya haraka.