Hospitali ya Mkongani yapandishwa hadhi

Rais Ruto aliongoza shughuli hiyo akiwa na viongozi kadhaa kama Gavana wa Kwale Fatuma Achani na waziri wa Afya Deborah Barasa.

Marion Bosire
3 Min Read

Rais William Ruto na Gavana wa Kwale Fatuma Achani hii leo waliongoza shughuli ya kupandishwa hadhi kwa hospitali ya Mkongani hadi level 4, ufunguzi rasmi wa chumba cha upasuaji, wadi ya kawaida na uzinduzi wa jengo la X-ray.

Ukarabati pamoja na miradi mipya hospitalini humo vilivyotekelezwa na serikali ya kaunti ya Kwale, vinatarajiwa kuondolea wakazi mzigo wa kusafiri mbali kutafuta matibabu maalumu.

Hospitali ya Mkongani level 4 sasa itakuwa ikitoa huduma spesheli za wataalamu kwa kina mama wajawazito wapatao 1500 kila mwezi, kuingilia kati mapema katika safari ya ujauzito na hivyo kupunguza vifo vya kina mama hao.

Taasisi hiyo ambayo inahudumia watu wapatao elfu 10 katika vijiji vinane ambavyo ni Mkongani A, Mkongani B, Vumirira, Goyo na vingine sasa itatoa huduma za upasuaji kama wa kujifungua, wa ngiri na wa kiambatisho.

Uwepo wa chumba cha upasuaji pamoja na maafisa wa afya katika hospitali hiyo ya Mkongani una maana kwamba huduma za upasuaji zitatolewa papo hapo kinyume na awali ambapo wagonjwa walikuwa wakitumwa kwenye hospitali ya Kwale umbali wa kilomita 40.

Akizungumza na wakazi wa Mkongani katika kaunti ndogo ya Matuga, Rais Ruto alithibitisha kujitolea kwa serikali yake kuboresha huduma za afya kote nchini kupitia ushirikiano na Serikali za Kaunti.

Rais alihimiza wakazi kujisajili kwa Mamlaka ya Huduma za Afya ya Jamii (SHA) ambayo itapunguza mzigo wa kulipa bili kubwa za matibabu kwa familia zao.

“Nitampa milioni 30 Gavana wenu Fatuma Achani ili kusaidia kuboresha hospitali hii ili wakazi wapate huduma bora,” aliongeza Rais Ruto.

Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Kwale, Fatuma Achani, alisema Serikali yake imeboresha hospitali za Kwale, Lungalunga, Samburu na Kinango hadi kiwango cha 4, huku Msambweni ikiboreshwa kuwa hospitali ya rufaa kwa matibabu maalum.

Achani aliongeza kusema kuwa utawala wake umeleta huduma za afya karibu na mwananchi kupitia ujenzi na uwekaji wa vifaa vya afya pamoja na ajira ya wataalamu wa afya wa kutosha.

“Hadi sasa tumekuwa tukijenga zaidi ya vituo vya afya 178 na kuajiri zaidi ya wafanyakazi wa afya 1800 na Wafanyakazi wa Afya ya Jamii zaidi ya 1600 kote katika Kaunti ili kuhakikisha wakazi wanapata huduma za afya kwa urahisi,” aliongeza.

Mbunge wa Matuga, Kassim Tandaza alipongeza viongozi wa Serikali ya Kaunti kwa jitihada kubwa walizofanya kuboresha sekta ya afya tangu kuanzishwa kwa ugatuzi.

Walioshuhudia shughuli hiyo ni pamoja na Waziri wa Afya Deborah Mulongo, Waziri wa Michezo Salim Mvurya, Naibu Gavana Chirema Kombo, Katibu Mkuu wa Kaunti Sylvia Chidodo, Naibu Msemaji wa Serikali Mwanaisha Chidzuga, wawakilishi wadi wa Kaunti la Kwale, Maafisa Wakuu, Mbunge wa Matuga Kassim Tandaza, Spika wa Bunge la Kaunti Seth Mwatela, na viongozi wa Serikali za Kitaifa na Kaunti.

Share This Article