Kongamano la Trace lilianza jana Februari 24, 2025 katika hoteli ya kifahari ya Mora Resort, katika kisiwa cha Zanzibar nchini Tanzania.
Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi alifungua rasmi kongamano hilo ambalo litahitimishwa kwa tuzo za Trace kesho Februari 26, 2025 katika eneo hilo hilo.
Katika hotuba hiyo, Mwinyi alisema kwamba serikali itaendelea kuwaunga mkono wasanii, “kwa kuwa ni muhimu katika kukuza utalii, uwekezaji, na urithi wa utamaduni miongoni mwa jamii.”
Kiongozi huyo aliwarai waandaaji na washiriki wa tamasha hilo kuwa, mbali na kufurahia muziki, litumike pia kujenga ushirikiano, umoja na uhusiano mzuri miongoni mwa wasanii.
Hii ndio mara ya kwanza Zanzibar inakuwa mwenyeji wa Tamasha la Tuzo za Muziki za Kimataifa za Trace linalofanyika katika Hoteli ya Kitalii ya Mora, Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Wasanii mbali mbali ambao wameteuliwa kuwania tuzo za mwaka huu za Trace waliwasili kisiwani humo jana Jumatatu huku wanaotumbuiza wakitangulia kwa ajili ya maandalizi.
Msanii wa pekee wa Kenya aliyeteuliwa kuwania tuzo hizo mwaka huu Bien Aime wa kundi la muziki la Sauti Sol naye yuko katika kongamano hilo.
Anawania tuzo ya msanii bora wa eneo la Afrika mashariki na ni mmoja wa watumbuizaji pia.
Wasanii wengi wa Tanzania wameteuliwa kuwania tuzo hizo labda kutokana na ukweli kwamba wao ndio waandalizi wa makala ya mwaka huu.