Seneta Khalwale aondoa mswada wa kudhibiti wanabodaboda

Martin Mwanje
1 Min Read
Dkt. Boni Khalwale - Seneta wa Kakamega

Seneta wa kaunti ya Kakamega Dkt. Boni Khalwale ameondoa mswada tata aliokuwa ameuwasilisha bungeni kuhusu udhibiti wa sekta ya biashara ya usafiri wa bodaboda.

Hatua hiyo inajiri baada ya wahudumu wengi wa bodaboda kupinga mswada huo kwa madai kwamba ungeathiri pakubwa biashara yao.

Akiwahutubia wanahabari huko Kakamega, Dkt. Khalwale amedai kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwachochea waendeshaji wa bodaboda dhidi ya mswada huo.

Seneta huyo ameeleza kuwa tayari ameandika barua rasmi ya kuondoa mswada huo kutoka Bunge la Seneti na Bunge la Taifa.

Wakosoaji wa Dkt. Khalwale wanamtuhumu kwa kuandaa mswada huo bila kuwahusisha washikadau wa sekta hiyo.

Miongoni mwa mambo mengine, mswada huo ulikuwa umependekeza kuwa wanabodaboda wasibebe uzito unaozidi kilo 50.

Wanabodaboda nchini Kenya wanafahamika kwa kubeba vitu vyenye uzito kupitiliza.

Share This Article