Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) itahakikisha kila Mkenya anapata huduma bora za matibabu na hivyo kuleta mwamko mpya katika sekta ya afya nchini.
Rais William Ruto amesema mfumo huo, ukiungwa mkono na wahudumu wa afya ya jamii, utaichochea nchi hii kuelekea upatikanaji wa afya kwa wote (UHC).
“Tunatoa wito kwa Wakenya kujiandikisha na kunufaika kutokana na mfumo huo wenye kuleta mabadiliko katika utoaji wa huduma za afya,” alirai Rais Ruto.
Alitoa wito huo leo Jumatano wakati akiweka jiwe la msingi la jengo la eksirei na kufungua rasmi jengo la kufanyia upasuaji katika hospitali ndogo ya Mkogani, kaunti ya Kwale.

Hospitali hiyo imepandishwa hadhi kutoka Ngazi ya 3 hadi 4 katika hatua inayotazamiwa kuboresha utoaji huduma kwa wakazi wa eneo hilo.
Wakenya zaidi ya milioni 19 wamejiandikishwa kwenye mfumo wa SHA uliochukua mahali pa iliyokuwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF).
Hata hivyo, Wakenya wamelalamikia huduma mbovu zinazotolewa na SHA wakisema wanalazimika kutumia fedha zao kugharimia matibabu.
Wakiwa kwenye mkutano mjini Naivasha wiki chache zilizopita, wabunge pia walilalamikia huduma mbovu zinazotolewa na SHA na kutaka Wizara ya Afya kujibidiisha kuuboresha mfumo huo.
Hospitali za binafsi zimetangaza kusitisha utuamiaji wa mfumo huo zikilalamikia kutolipwa malimbikizi ya fedha zinazodai.
Serikali inasema inafanya kazi usiku na mchana kuboresha utendakazi wa mfumo huo.