Mawakili wa mwanamuziki P.Diddy wamechukua hatua ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga vibali walivyopatiwa na mahakama vya kutekeleza misako kwenye makazi yake na kudadisi vitendo vyake mitandaoni.
Wanadai kwamba maafisa hao wa upelelezi walitoa taarifa za uongo walipotuma maombi ya vibali hivyo.
Wanasheria hao waliwasilisha stakabadi za kesi hiyo Jumapili Februari 23, 2025 wakitaka jaji akandamize ushahidi wote uliokusanywa wakati wa misako hiyo kwani maafisa wa serikali waliwasilisha habari potovu.
Kundi hilo la wanasheria wa Diddy, linasema kwamba maafisa hao walikuwa na ushahidi mbali mbali unaoashiria kwamba lau mmoja wa waathiriwa alishiriki sherehe za kingono za Diddy kwa hiari.
Katika stakabadhi za mahakama, maafisa wa upelelezi wanaelezea sherehe hizo za Diddy kuwa za siku kadhaa na zilihusisha vitendo vya kujamiana kati ya Diddy,mwanamke na makahaba wa kiume wengine ambao walisafirishwa kutoka majimbo ya mbali.
Mawakili wa Diddy hata hivyo wanasisitiza kwamba baadhi ya mawasilisho ya maafisa wa upelelezi hayakuwa ya kweli na waliyatoa kimakusudi kwa nia ya kupotosha.
Kulingana nao, uongo wa wapelelezi ulifanikiwa kwani walipatiwa vibali vya kufanya misako katika nyumba kadhaa anazomiliki Diddy kabla ya kuvujisha habari mbaya.
Jambo lingine ambalo wanataka lishughulikiwe na mahakama ni hatua ya walalamishi kumotishwa na pesa ambazo wanaweza kupata kutoka kwa Diddy ndiposa wakajitokeza.
Kesi ya Diddy iliangaziwa sana mwaka jana wakati maafisa wa upelelezi walivamia makazi yake ya New York, Miami na Los Angeles ambapo walifanya misako.
Baada ya misako, Diddy alikamatwa katika hoteli moja ya New York mwezi Septemba na amenyimwa dhamana mara kadhaa.