Rais William Ruto ameomboleza kifo cha Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati.
“Nimepokea taarifa za kufariki kwa Mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati kwa huzuni mkubwa,” alisema Rais Ruto kwenye risala zake za rambirambi.
“Chebukati alikuwa kiongozi mwenye msimamo na mwerevu aliyetumikia taifa kwa uadilifu. Kifo chake ni pigo kwa nchi yetu.”
Chebukati aliyekuwa na umri wa miaka 63 alifariki jana Alhamisi jioni wakati akitibiwa katika hospitali moja jijini Nairobi.
Marehemu aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa IEBC mnamo mwezi Januari mwaka 2017.
Atakumbukwa kwa kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 na 2022, chaguzi ambazo zilikumbwa na utata hususan kuhusiana na matokeo ya urais.
Alihudumu kwa wadhifa huo kwa vipindi viwili akiwa pamoja na Makamishna Prof. Abdi Guliye na Boya Molu.
Wote hao waliondoka kwenye tume huyo mwezi Januari mwaka 2023 baada ya muhula wao wa kuhudumu kumalizika.
Makamishna wengine ambao ni Juliana Cherera, Francis Wandera, Irene Masit na Justus Nyang’aya (maarufu kama Cherera 4) walijiuzulu kabla ya kumalizika kwa muhula wao wa kuhudumu.
Wanne hao walichukua hatua hiyo kutokana na utata uliogubika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.