Maafisa 13 wa polisi, afisa wa Idara ya Taifa ya Ujasusi (NIS) pamoja na mlinzi wa Shirika la Wanyamapori nchini (KWS) wameshtakiwa katika Mahakama Kuu ya Kiambu kuhusiana na mauaji ya Mkenya mmoja na raia wawili wa India.
Walioshtakiwa ni pamoja na Peter Muthee Gachiko (Inspekta Mkuu wa Polisi), James Kibosek, (Inspekta wa Polisi), na Makoplo Joseph Kamau Mbugua, David Chepchieng, Joseph Mwenda, John Mwangi na Hillary Limo. Maafisa wengine Makoplo Stephen Luseno, Simon Muhuga, Paul Njogu, Boniface Otieno, Elkana Njeru na Fredrick Thuku.
Maafisa wengine walioshukishwa kizimbani ni John Wanjiku Macharia (NIS) na Michael Kiplangat (KWS).
Wote hao wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya Mohammed Zaid Sami Kidwali na Zulfiqar Ahmed Khan ambao ni raia wa India na Mkenya Nicodemus Mwania Mwange.
Mahakama iliambiwa kwamba usiku wa Julai 22 na 23, 2022 karibu na hoteli ya Ole Sereni kwenye barabara ya Mombasa Road, kaunti ya Nairobi, kwa pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani, washtakiwa waliwateka nyara na kuwaua watatu hao.
Walishtakiwa walikanusha mashtaka dhidi yao walipofikishwa mbele ya Jaji Abigael Mshila.
Maafisa hao watasalia kizuizini hadi kesi hiyo itakapotajwa Machi 20 mwaka huu.